1. Ongea na Mungu
Jambo la kwanza kufanya ni kuongea na Mungu. Unaweza kukiri kwake kwamba umemwasi na unastahili adhabu, halafu na umwombe akusamehe dhambi zako zote kwa sababu Yesu alikufa kwa niaba yako. Umwombe Mungu akusaidie kuachana na uasi dhidi yake na kujitahidi kuishi chini ya mamlaka ya Bwana Yesu Kristo. Sasa, unaweza kuomba kama hivi:
Mungu Baba
Najua sistahili kuwa mbele yako. Sistahili zawadi yako ya uzima wa milele. Nimekukosea kwa kuasi dhidi yako na kukataa mapenzi yako. Najutia makosa yangu na ninasikitika. Nahitaji msamaha wako.
Asante kwa kumtuma mwanao Yesu afe kwa ajili yangu ili nisamehewe. Asante kwamba alifufuka katika wafu ili anipe uzima mpya.
Naomba unisamehe na unifanye upya, ili niweze kumtii Yesu na kumheshimu kama mtawala wangu. Amina.
2. Mtii Yesu
Baada ya kuongea na Mungu ukiungama makosa yako na kuomba msamaha (kama ile sala hapo juu) hatua ya pili inafuata. Basi ni vema kutekeleza katika maisha yako ombi la kufanywa upya. Ni muhimu kuanza upya na kumwishia Yesu Kristo kwa utii na heshima.
Inatubidi kubadilisha mambo katika sehemu zote za maisha yetu. Hivyo inabidi tabia zile za uasi kuachana nazo (kama uchoyo, hasira, ubinafsi, na kadhalika). Lakini pia kuna tabia mpya zinazompendeza Mungu unapaswa kuzichukua na kuzifanyia kazi (kama ukarimu, fadhili, upendo, na uvumilivu).
Hatua hii ya pili itaendelea kwa maisha yako yote, lakini Mungu atakuwa pamoja nawe siku zote. Mungu ataendelea kusema nawe kila unaposoma neno lake, yaani Biblia. Mungu ataendelea kukusikiliza na kukusaidia kila unapomwomba. Kwa Roho wake anayekaa ndani yako, Mungu anakufanya upya na anakuwezesha ili uishi katika njia yake. Mungu atakukutanisha pamoja na Wakristo wengine ili wakuhimize na kukutia moyo.
Hivyo hatua ya pili ni kumtii Yesu Kristo na kuanza kuishi chini ya mamlaka yake Yesu mtawala wako.
3. Mwamini Yesu
Hatua ya tatu pia inaendelea. Lazima kuendelea kuweka imani yako katika Yesu.
Kuna njia moja tu na pekee kwa mtu kupata amani kwa Mungu. Unaweza kusamehewa na kupatanishwa na Mungu kwa sababu ya Yesu tu (na kifo chake na ufufuo). Mtu anaokolewa kwa kumwamini Yesu tu. Msingi wa wokovu wote na maisha yote ni Yesu na kifo chake na ufufuo wake. Basi kama Wakristo wote, japo unataka kuishi kwa njia ya Mungu, bado utakosa na kutenda vibaya. Lakini hata hivyo msingi wa wokovu ni ule ule. Sisi sote hatuna budi siku zote kuamini na kumtegemea Yesu na kifo chake msalabani kuwa ndiyo sababu pekee ya kusamahewa.
Hatupaswi kamwe kuacha kumtegemea Yesu peke yake awe namna ambayo tumesamehewa na kupewa uzima wa milele.
Ikiwa utachukua hatua hizi, unaweza kuwa na uhakika kuwa Mungu amekusamehe makosa na dhambi zako zote na pia amekupa uzima mpya.
Lakini ikiwa bado haujamwitikia Mungu kwa njia hii, unaweza kuwa na uhakika kuwa ghadhabu ya Mungu inabaki juu yako.
Ni kama umefika njiapanda katika barabara. Kuna njia mbili tu za kuishi. Sisi sote hatuna budi kuchagua kati ya njia hizi mbili.